Akizunguza kwa huzuni katika hotuba aliyoitoa akiwa White House majira ya jioni, Biden alisema kundi la Islamic State tawi la Afghanistan liitwalo ISIS K ndilo lilihusika na mashambulizi ambayo yaliuwa wanajeshi 13 wa Marekani na darzeni za raia wa Afghanistan,
Biden aliyasema hayo huko ikithibitishwa kwamba pamoja na raia hao wa Marekani, zaidi ya Waafghanitan 60 walipoteza maisha yao kwenye mashambulizi hayo.
"Hatutawasamehe na hatutasahau," Biden alisema wakati wa hotuba yake kabla ya kujibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari.
Alisema hakuna ushahidi kwamba washambuliaji walikula njama na Taliban ambao wanaidhibiti nchi.
Karibu Wamarekani elfu moja na Waafghanistan wengi wameshindwa namna ya kuondoka mjini Kabul.
Zaidi ya watu laki moja wamekwisha ondolewa nchini Afghanistan kufikia sasa.
Mapema Alhamisi, milipuko miwili karibu na uwanja wa ndege wa Kabul, iliwaua wanajeshi wa Marekani na Waafghanistan waliokuwa wamekusanyika eneo hilo, wakijaribu kuondoka nchini Afghanistan.
Kamanda wa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan, Jenerali Frank McKenzie alisema katika mkutano wa waandishi wa habari kwamba, wanafuatilia matukio mjini Kabul kwa karibu.
Kundi la kigaidi la Islamic State limedai kuhusika na shambulio hilo.
McKenzie alisema, wataendelea kutekeleza jukumu lao kuu, ambalo ni kuwandoa Wamarekani na raia wengine nchini Afghanistan.
Amesema ISIS haitawazuia kufanikisha kazi yao.
Akizungumzia kuhusu mlipuko wa kwanza, afisa wa Taliban ameiambia Sauti ya Amerika kwamba, mshambuliaji wa kujitoa muhanga amejilipua katika eneo ambapo kulikuwa kumekusanyika watu wengi, mkiwemo wanawake.
Milipuko hiyo ilitokea saa kadhaa baada ya serikali za magharibi kutoa onyo juu ya tishio la shambulio la kigaidi kwenye uwanja wa ndege na kuwaomba watu waliokuwa wamekusanyika eneo hilo wakisubiri kuondolewa nchini Afghanistan, kujielekeza kwenye eneo salama.
Kufuatia milipuko hiyo, ubalozi wa Marekani mjini Kabul, umewataka raia wa Marekani kutoenda kwenye uwanja wa ndege na kuepuka milango ya uwanja huo