Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Novemba 24, 2024 Local time: 22:03

Biden aahidi kumteua mwanamke kama makamu wake


Makamu wa Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden (kushoto) na Seneta wa jimbo la Vermont Bernie Sanders wakati wa mdahalo uliofanyika mjini Washington DC tarehe 15 Machi, 2020.
Makamu wa Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden (kushoto) na Seneta wa jimbo la Vermont Bernie Sanders wakati wa mdahalo uliofanyika mjini Washington DC tarehe 15 Machi, 2020.

Makamu wa rais wa zamani wa Marekani Joe Biden Jumapili usiku aliahidi kwamba iwapo atapata uteuzi wa chama cha Demokratik wa kuwania urais kwenye uchaguzi ujao wa mwezi Novemba, atamteua mwanamke kama mgombea mwenza.

Biden alikuwa akizungumza wakati wa mdahalo kati yake na mgombea mwingine wa tikiti ya chama cha Demokratik, Seneta Bernies Sanders, uliofanyika mjini Washington DC, na kupeperushwa moja kwa moja na mashirika ya habari ya CNN na Univision.

"Kuna wanawake wengi ambao wanahitimu hata kuwa rais. Naahidi sasa hivi kwamba nitamteua mwanamke kama makamu wangu," alisema.

Kwa upande wake, Sanders, ambaye ni seneta wa jimbo la Vermont, alionekana kusita alipoulizwa kama angetoa ahadi sawa na hiyo ya Biden, akisema tu kwamba lililo muhimu ni kumteuea mtu ambaye ana maono sawa naye.

Hata hivyo, Sanders aliongeza kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba yeye pia atamteua mwanamke.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa wawili hao kukutana peke yao kwenye mdahalo kufuatia kujiondoa kwa wenzao, waliokuwa wanawania tikiti hiyo, na ambao waliamua kufanya hivyo baada ya kutopata kura za kutosha kuwawezesha kuwa na uhakika wa kushinda tikiti hiyo.

Seneta wa Massachusetts Elizabeth Warren, Seneta Kamala Harris wa California na mwenzao wa Minnesota, Emi Klobuchar, wanatajwa na wachambuzi kama kati ya wanawake ambao huenda wakapewa nafasi hiyo.

Wanawaka hao wote wameng'atuka baada ya kupambana vikali katika chaguzi za awali za chama cha Demokratik, ambazo zimekuwa zikifanyika tangu tarehe 3 mwezi Februari.

Aliyekuwa mgombea wa ugavana katika jimbo la Georgia, Stacey Adams, pia anatajwa kama mwenye nafasi nzuri ya kuwa mgombea mweza wa Biden au Sanders.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mdahalo kama huo kufanyika bila mashabiki kuwa ukumbini kama njia ya kukabiliana na uwezekano wa kuenea kwa virusi vya homa ya Coronavirus.

Sanders na Biden pia waliahidi kwamba licha ya tofauti zao za kisera, iwapo mmoja wao hatapata uteuzi wa chama, basi atamuunga mkono mwenzake "ili kumng'oa mamlakani Rais Donald Trump wa chama cha Republican."

XS
SM
MD
LG