Mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu -ICC ameisihi serikali ya mpito ya Sudan kuwakabidhi washukiwa wanaotafutwa kwa uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari katika mzozo wa Darfur.
Mwendesha mashtaka wa ICC Fatou Bensouda aliwasili katika mkoa wa magharibi wa Sudan wa Darfur Jumamosi ili kukutana na mamlaka na jamii zilizoathiriwa katika eneo hilo.
Miongoni mwa wale wanaotafutwa na mahakama ya kimataifa ni Rais wa zamani wa Sudan Omar al-Bashir, ambaye amekuwa gerezani mjini Khartoum tangu kuondolewa kwake madarakani mwezi Aprili 2019.
Serikali ya mpito ya Sudan hapo awali ilisema kwamba washukiwa wa uhalifu wa kivita pamoja na al-Bashir watahukumiwa kwenye mahakama ya ICC , lakini mahali pa kufanyika kwa kesi ni suala la mashauriano na mahakama hiyo iliyo na makao yake mjini Hague.