Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 27, 2024 Local time: 08:32

Benki ya dunia: Uvamizi wa Russia dhidi ya Ukraine tayari umesababisha hasara ya dola bilioni 60


Jengo lililoharibiwa wakati wa mapigano katika mji wa bandari wa Mariupol, April 13, 2022. Picha ya AP
Jengo lililoharibiwa wakati wa mapigano katika mji wa bandari wa Mariupol, April 13, 2022. Picha ya AP

Uharibifu wa majengo na miundombinu ya Ukraine kutokana na uvamizi wa Russia umefikia hasara ya takriban dola bilioni 60 na utaongezeka zaidi kadri vita vinavyoendelea, Rais wa Benki ya dunia David Malpass amesema Alhamisi.

Malpass ameuambia mkutano wa Benki ya dunia kuhusu mahitaji ya msaada wa kifedha wa Ukraine kwamba makadirio ya awali ya gharama “finyu” za uharibifu hayajumuishi gharama za kiuchumi zinazoongezeka za vita vya Ukraine.

Malpass amesema “ Vita bado vinaendelea, kwa hivyo gharama zinaongezeka.”

Rais wa Ukraine akihotubia kwa njiya ya mtandao mkutano huo uliofanyika mjini Washington , ameelezea gharama kubwa zaidi na mahitaji ya kifedha. Amewambia washiriki katika matamshi yaliyotafsiriwa kuwa Ukraine inahitaji dola bilioni 7 kwa mwezi kufidia hasara ya kiuchumi iliyosababishwa na uvamizi wa Russia dhidi ya nchi yake.

Tutahitaji mabilioni ya dola kuijenga upya nchi baadaye,” Zelensky amesema.

Amesema jumuia ya kimataifa inatakiwa kuiondoa Russia mara moja kwenye taasisi za kifedha za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Benki ya dunia na Shirika la kimataifa la fedha(IMF) na nyinginezo, na kusema nchi zote “lazima ziwe tayari mara moja kuvunja uhusiano wote na Russia.”

Mkutano huo ambao ulifanyika kando ya mikutano ya IMF na Benki ya dunia ya majira ya baada ya msimu wa baridi ulijumuisha maafisa wa fedha kutoka nchi kadhaa, akiwemo waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen, ambaye awali amesema Marekani itaongeza mara dufu ahadi yake ya msaada wa moja kwa moja usiokuwa wa kijeshi kwa Ukraine hadi dola bilioni 1.

“Nimejitolea kufanya kazi na washirika wetu kusaidia katika mahitaji ya kiuchumi ya Ukraine kwa muda mfupi na mrefu. Katika mkutano huo, nimeelezea ahadi ya ufadhili mwingine wa Marekani wa dola milioni 500 ili kuisaidia Ukraine kuendelea na shughuli muhimu za serikali, kama vile mishahara, pensheni na program nyingine za msaada wa kijamii zenye umuhimu ili kuepuka kuzorota kwa hali ya kibindamu nchini Ukraine,” amesema Yellen.

Waziri mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal, ambaye alihudhuria mkutano huo ana kwa ana, amesema pato la taifa la Ukraine linaweza kuporomoka kwa asilimia 30 hadi asilimia 50, na hasara ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja ni jumla ya dola milioni 560 kufikia sasa.

Kiwango hicho ni zaidi ya mara tatu ya ukubwa wa uchumi wa Ukraine, ambao ulikuwa sawa na dola bilioni 155.5 mwaka wa 2020, kulingana na takwim za Benki ya dunia.

XS
SM
MD
LG