Lengo kuu la mkutano huo wa Baraza la usalama la Umoja wa mataifa ni kuhusu shambulio la kombora kwenye jengo kubwa la maduka ya biashara katikati mwa jiji la Kremnchuk, amesema msemaji wa ujumbe wa Albania, ambao unaongoza uenyekiti wa Baraza hilo kwa sasa.
Mashambulizi ya makombora mjini kote Kyiv siku ya Jumapili, dhidi ya jengo la makazi ya watu, yatajadiliwa pia kwenye mkutano huo, msemaji huyo amesema.
Watu 13 wamethibitishwa kuuawa katika shambulio la Kremenchuk, ambalo limelaaniwa na Umoja wa mataifa na viongozi wa dunia.
Maafisa wa Ukraine wameishtumu Moscow kulenga raia baada ya ripoti ya mashambulizi mengine mawili mashariki mwa nchi jana Jumatatu ambayo yaliua watu 12.
Russia ambayo ilianza uvamizi dhidi ya Ukraine mwezi Februari mwaka huu, imekanusha tuhuma kwamba mashambulizi hayo ya Jumapili kwenye mji mkuu wa Ukraine yalilenga makazi ya watu, ikisema ilikuwa inalenga kiwanda cha silaha.