Baba mtakatifu benedict amelaani mashambulizi ya siku ya krismas kwenye makanisa nchini Nigeria, na kuyaita ni kitendo cha kipuuzi. Wanamgambo wa kundi lenye msimamo mkali wa kiislamu boko haram wamedai kuhusika na mabomu hayo.
Kwa mwaka wa pili mfululizo, kundi lenye msimamo mkali la boko haram limefanya mashambulizi siku ya krismas kwenye nyumba za ibada za wakristo nchini Nigeria. Kundi hilo limedai kuhusika na ulipuaji mabomu kwenye makanisa matatu siku ya Jumapili wakati wa sikukuu ya krismas.
Majeshi ya Nigeria pia yamelilaumu kundi hilo kwa milipuko mingine miwili kaskazini mwa nchi hiyo.
Akiongea kupitia dirishani upande unaoangalia eneo la saint peters square Jumatatu, baba mtakatifu alilaani mashambulizi hayo ambayo yameua dazeni ya watu.
Baba mtakatifu amesema amesikitishwa sana na mashambulizi hayo, ambayo kwa mwaka mwingine tena, yamefanyika siku ambayo Yesu amezaliwa, na kusababisha maumivu na maombolezo katika baadhi ya makanisa nchini Nigeria. Baba mtakatifu alielezea ukaribu wake na jamii ya wakristo na wote ambao wameathiriwa na kitendo hiki cha kipuuzi.