Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Januari 03, 2025 Local time: 10:42

Baadhi ya vipengele vyenye ubishani mkubwa katika mapendekezo ya katiba Kenya


Mabishano makali yamejitokeza kutokana na mapendekezo ya katiba mpya inayopigiwa kura Augusti 4 nchini Kenya. Hivi ni baadhi ya vipengele ambavyo vimezusha ubishani mkubwa, hamasa na uhasama baina ya wanaounga mkono na wanaopinga.

Utoaji mimba: Kinasema maisha ya binadamu huanza mimba inapotungwa na kila mtu ana haki ya kuishi. Vile vile, kinasema kuwa utoaji mimba ni haramu. Hata hivyo, mtaalamu wa afya anaweza kuamua kukatiza mimba iwapo afya na maisha ya mama mjazito yako hatarini. Wanaopinga mapendekezo ya Katiba wanasema wataalamu wa afya watatumia kipengele hiki kuwa kisingizio cha kujiingiza katika biashara ya utoaji mimba wakijua hawatakabiliwa kisheria.

Mahakama za Kadhi: Kinasema Mahakama za Kadhi zinaruhusiwa kushughulikia masuala ya ndoa, talaka na urithi ikiwa wahusika wote ni Waislamu na wanataka kwa hiari mambo yao yasimamiwe na mizozo yao isuluhishwe na Mahakama za Kadhi. Ikiwa wote ni Waislamu na mmoja hataki kwenda kwa Kadhi, basi wanakwenda katika mahakama za kawaida. La ziada ni kuwa hukumu zinazotolewa na Mahakama za Kadhi zinaweza kukatiwa rufaa katika mahakama kuu za kiserikali ikiwa mhusika mmoja hakuridhika. Kipengele hiki kinapingwa na viongozi wa makanisa wakisema kinapendelea dini moja ilhali utangulizi wa Katiba Inayopendekezwa unasema Kenya si taifa la kidini. Wanasema ikiwa Waislamu wanapewa mahakama zao kwa sababu ni miongoni mwa makundi ya wachache nchini, hali itakuwaje wakiongezeka, hasa ikizingatiwa ili kubadili hata aya moja ya Katiba hii ni lazima kura ya maamuzi iandaliwe.

Uraia: Kinasema mtoto yeyote atakayepatikana nchini bila wazazi, mradi awe na umri wa chini ya miaka minane, atachukuliwa kuwa Mkenya. Wanaopinga kipengee hiki wanasema huenda Kenya ikaja kutawaliwa na wageni, hasa ikizingatiwa eneo la Maziwa Makuu halikosi wakimbizi kutokana na mizozo ya mara kwa mara. Wanahofia kuenda watu kutoka nchi jirani zenye migogoro wanaweza kuelekeza watoto wao mipakani wakiwa na ushauri kuwa wakiulizwa waseme hawajui wazazi wao, wakitaka wapate uraia wa Kenya.

Ardhi: Hiki kinasema ardhi za jamii (kwa mfano jamii za wafugaji ambazo hazipewi hati miliki kwa sababu huhamahama kutafuta maji na malisho) hazitatwaliwa kinyume cha sheria. Wanaopinga wanasema kipengele hiki kitagawanya Wakenya kwa misingi ya kikabila kwani itakuwa vigumu kueleza jamii ni nini, hasa ikizingatiwa kuna makabila mchanganyiko ambayo huishi maeneo mamoja.

Sheria na Mikataba Inayotiwa Saini katika Makongamano ya Kimataifa: Hiki kinasema kuwa mikataba yoyote itakayotiwa saini katika makongamano ya kimataifa, na Serikali ya Kenya iwe na mwakilishi, itajumuishwa katika sheria za nchi bila hata kujadiliwa bungeni. Wanaopinga Katiba Inayopendekezwa wanasema kipengele hiki kitatumika kuleta sera mbovu za kigeni nchini, kwamba kuna hatari ya mila na desturi zisizo za Kiafrika kama vile ushoga zitakubalika bila hiari ya Wakenya.

Uhuru wa Vikosi vya Usalama Kuwa na Vyama vya Wafanyikazi: Katiba Inayopendekezwa inasema kuwa kila Mkenya (mfanyakazi) ana haki ya kushiriki maandamano akidai matakwa yake yatimizwe. Lakini inasema wazi kuwa haki hii haitafurahiwa na vikosi vya usalama. Hata hivyo, wanaopinga Katiba hiyo wanauliza vikosi vya usalama vitakuwa vya kutekeleza majukumu gani. Wanahofia huenda ikawa rahisi kwa majeshi kupindua Serikali wakiwa na kiongozi mmoja wa kisiasa (ikichukuliwa kuwa vyama vya wafanyakazi ni kama vya kisiasa kwa sababu vyeo hugombewa) ambaye atakuwa akitoa amri na wenzake wakitii, hasa kuhusu maslahi yao kazini.

XS
SM
MD
LG