Kiongozi wa Myanmar, Aung San Suu Kyi, siku ya Alhamisi alikutana na viongozi wa bunge la Marekani, siku moja tu baada ya rais Barack Obama kutangaza kuwa serikali yake iko tayari kuondoa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa ratiba rasmi, Aung San Suu Kyi, ambaye yuko ziarani hapa Marekani, alitarajiwa kukutana na kiongozi wa wachache katika bunge la Congress, Nancy Pelosi na kiongozi wa waliowengi katika seneti, Mitch McConnell, na vile vile kuhudhuria dhifa itakayoandaliwa na viongozi wa kibiashara na hatimaye kufanya kikao cha maswali na majibu na wanafunzi wa shule ya upili ya Washington.
Huenda pia Aung San Suu Kyi akajaribu kuwashawishi wabunge wenye ushawishi mkubwa bungeni kwamba huu ni wakati mwafaka kuondoa vikwazo hivyo vya kiuchumi dhidi ya nchi yake.