Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 21, 2024 Local time: 17:37

Umoja wa Afrika waipinga ICC


Wakuu wa nchi za Afrika pamoja na wawakilishi katika mkutano wa AU huko Malabo nchini Eguatorial Guinea, ambao ulizungumzia kwa kina mgogoro wa Libya.
Wakuu wa nchi za Afrika pamoja na wawakilishi katika mkutano wa AU huko Malabo nchini Eguatorial Guinea, ambao ulizungumzia kwa kina mgogoro wa Libya.

Umoja wa Afrika-AU umesema hautashirikiana na mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC kumkamata kiongozi wa Libya Moammar Ghadafi kufuatia hati iliyotolewa na mahakama hiyo dhidi ya kiongozi huyo.

Aidha Umoja wa Afrika unasema kutolewa kwa hati ya kukamatwa kwa kiongozi huyo kunavuruga juhudi za kutafua ufumbuzi wa mzozo wa Libya. Kamishina wa Umoja wa Afrika Jean Ping anasema mahakama hiyo inabagua, kwa sababu inawafuata tu wale wanaodaiwa kufanya uhalifu barani Afrika, na kupuuzia wanaofanya uhalifu wa kivita katika dola zenye nguvu za Magharibi kama inavyobainika nchini Iraq , Afghanistan na Pakistan.

Lakini naibu mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya ICC mzaliwa wa Gambia Fatou Bensouda, anasema madai hayo hayatilii maanani idadi ya waafrika wanaotafuta msaada wa mahakama hiyo ya ICC. ICC ilitoa hati ya kukamatwa kwa Rais wa Sudan Omar al-Bashir takriban mwaka mmoja uliopita lakini mpaka wakati huu ameweza kusafiri kutoka nchi yake kuingia nchi nyingine za Afrika akiwa huru.

Lawama dhidi ya ICC kwamba inawalenga viongozi wa Afrika ilitolewa pia na wakili mtetezi katika kesi dhidi ya aliyekuwa Rais wa Liberia Charles Taylor, bwana Courtney Griffiths. Griffiths aliiambia mahakama hiyo kwamba ni aibu kwa waendesha mashitaka katika mahakama hiyo kukiuka sheria za kimataifa za uhalifu wa kivita kwa kuwa na msimamo wa kiukoloni mamboleo katika karne ya 21.

Kati ya nchi 53 za Afrika , nchi 31 zimetia saini mkataba wa Roma uliotoa mamlaka kwa mahakama ya ICC kusikiliza kesi za uhalifu wa kivita.

XS
SM
MD
LG