Polisi katika jimbo Colorado nchini Marekani wanasema watu 12 waliuwawa kwa kufyatuliwa risasi na wengine wasiopungua 38 kujeruhiwa katika tukio hilo lililotokea kwenye ukumbi wa sinema uliopo kwenye viunga vya Denver.
Maafisa wa polisi watu hao walikuwa wakijionea filamu ya “The Dark Knight Rises” kwenye mfululizo wa filamu mpya za Batman iliyotoka Ijumaa kwenye ukumbi wa mji wa Aurora ambapo kijana aliyevalia maski akiwa mbele ya ukumbi akiuangalia mkusanyiko wa watazamani alirusha gesi ya kutoa machozi na kuanza ufyatuaji risasi kiholela. Mashahidi walisema alimuuwa pia mtoto mmoja mdogo kwenye eneo la uzio wa kukagulia tiketi.
Polisi walimkamata mshukiwa wa tukio hilo muda mfupi baadaye kwenye eneo la kuegeshea magari nje ya ukumbi wa sinema. Walisema mshukiwa huyo kijana mwenye umri wa miaka 24 alikuwa na bunduki moja na bastola moja. Mkuu wa polisi katika mji wa Aurora, Daniel Oates aliwaambia waandishi wa habari kwamba tukio hilo lilimhusisha mtu mmoja pekee, akikanusha na ripoti za awali ambazo zilisema pengine kulikuwa na watu wengine walioshirikiana kwenye tukio hilo.
Mkuu huyo wa polisi alisema mshukiwa huyo aliwaambia wachunguzi kuwa alikuwa na milipuko kadhaa kwenye jengo la nyumba aliyopanga. Saa kadhaa baada ya tukio hilo kutokea mitandao ya televisheni za Marekani iliwaonyesha polisi wakiingiza chuma kirefu wakijaribu kuingia ndani ya nyumba yake.
Mshukiwa huyo ambaye yupo kizuizini alitoa taarifa kuhusu uwezekano wa kutokea milipuko kadhaa kwenye makazi yake anayoishi, Oates alisema. Katika taarifa iliyotolewa na White House, rais wa marekani Barack Obama anasema yeye na mke wake Michelle “wameshangazwa na wanahuzunika” kufuatia tukio hilo baya.