Kampuni ya mawasiliano ya simu ya Afrika Kusini imezindua app ya bure ya simu za mkononi kusaidia wahanga ambao ni walengwa wa unyanyasaji wa kijinsia, shida ambayo imeongezeka wakati wa kufungwa kwa shughuli za kiuchumi wakati wa janga la corona. App hiyo ilitengenezwa na Vodacom Afrika Kusini kwa kushirikiana na kampuni yake mama ya Uingereza na shirika la kutoa misaada la Hestia.
Jeanine mwanamke wa Afrika Kusini mwenye umri wa miaka hamsini na tatu ambaye hataki kutumia jina la familia yake alikuwa katika uhusiano wa manyanyaso kwa miaka miwili. Ilizidi kuwa mbaya wakati rafiki yake wa kiume alipopoteza ajira kwa sababu ya janga la corona na kumtolea hasira yeye.
Jeanine anakumbuka kwa uchungu nyakati zile za giza za uhusiano wake, bila kujua la kufanya.
Ili kumsaidia Jeanine na waathirika wengine wa unyanyasaji wa kijinsia, kampuni ya mawasiliano ya Afrika Kusini Vodacom, pamoja na kampuni yake mama ya Uingereza Vodafone na shirika la hisani Hestia, walizindua programu hiyo ya Bright Sky mwaka jana Novemba.
Afisa mtendaji wa Vodacom, Takalani Netshintenzhe, anasema Bright Sky inatoa huduma nyingi tofauti.
Vodacom inasema Bright Sky inaruhusu watumiaji kupata msaada bila unyanyapaa wa kulazimika kuiomba. Inasema app hiyo imepakuliwa takriban mara 1,000 nchini Afrika Kusini, ikisaidia wanawake wengi kama Jeanine.
App hiyo inakuja katika lugha tatu za Afrika Kusini - Kiingereza, Sesotho, na kiZulu.
Polisi wa Afrika Kusini wanasema kuwa unyanyasaji wa kingono unaripotiwa kila mwaka na umekuwa ukiongezeka tangu 2016 na umepita zaidi ya 53,000 mwaka jana.
Wanaharakati wanalaumu kufungwa kwa shughuli za kiuchumi na wanasema idadi halisi ya mashambulizi, pamoja na zile ambazo hazijaripotiwa, ni kubwa zaidi.