Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 19:52

Amnesty International: Serikali ya Tanzania inapandikizia wamaasai 25 mashtaka ya mauaji Loliondo


Wamaasai wanaoishi karibu na mbuga ya kitaifa ya Serengeti, Kaskazini mwa Tanzania. PICHA: AP
Wamaasai wanaoishi karibu na mbuga ya kitaifa ya Serengeti, Kaskazini mwa Tanzania. PICHA: AP

Shirika la Amnesty International limemuandikia barua rais wa Tanzania Suluhu Samia Hassan, kutaka oparesheni maalum ya kuwafurusha watu wa jamii ya wamaasai kutoka Loliondo katika mbuga ya taifa ya Serengeti, kusitishwa mara moja.

Katika barua hiyo, shirika la Amnesty International linamsihi rais Samia kutoa maagizo ya kuacha mara moja hatua ya kuwaondoa wamaasai kutoka sehemu hiyo hadi “wamaasai watakaporidhia bila kushurutishwa na waondoke kwa hiari yao baada ya mashauriano ya wazi na haki.”

Shirika hilo vile vile linataka uchunguzi huru na wa kina ufanyike kuhusu makabiliano yaliyotokea kati ya maafisa wa usalama na wamaasai mwezi Juni tarehe 9.

Licha ya serikali ya Tanzania kukosa kutoa taarifa kamili kuhusu idadi ya watu ambao wamekamatwa, kujeruhiwa au kuuawa wakati wa makabiliano kati ya maafisa wa usalama na wamaasai katika sehemu ya Loliondo, Amnesty International wanasema kwamba watu 25 wanazuiliwa na polisi kwa kupinga zoezi la serikali la kuwaondoa “katika ardhi yao ambayo wameishi kwa miaka mingi na ndipo wanapaita nyumbani,” na kuongezea kwamba “maafisa wa polisi walitumia nguvu katika kuwatawanya wamaasai waliokuwa wakiandamana kwa amani kupinga hatua ya maafisa wa usalama kuwafurusha makwao.”

Majina ya watu waliokamatwa

Shirika la AmnestyuInternational limesema kwamba lina ushahidi kwamba watu wafuatao wanazuiliwa na polisi:

Molongo Daniel Paschal, Albert Kiseya Selembo, Simeli Parmwati, Lekayoko
Parmwati, Sapati Parmwati Sirikoti, Ingoi Olkedenyi Kanjwel, Sangau Morongeti Ngiminiso, Morijoi Ngoisa Parmati, Morongeti Meeki Masako, Kamabatai Lulu, Moloimeti Yohana Saing’EU, Ndirango Senge Laisier, Joel Clemes Lessonu, Simon Naiam Orosikiria, Damiani Rago Laiza, Mathew Kursas Njausi, Taleng’o Twambei Leshoko, Kijoolu Kakenya Olojiloji, Shengena Joseph Killel, Kelvin Shaso Nairoti, Lekerenga, Fred Victor, Wilson Tiuwa Kilong, James Memusi Taki na wengine 5 ambao majina yao hayajatajwa.

Ripoti za walioshuhudia tukio la Juni 9 zinasema kwamba polisi, wanajeshi na walinzi wa mbuga waliwashambulia wamaasai kwa kutumia gesi ya kutoa machozi na risasi. Watu kadhaa walijeruhiwa na mtu mmoja (polisi) kufariki.

Wamaasai wengi walikimbilia nchi jirani ya Kenya kwa matibabu.

Waliokamatwa walifunguliwa mashtaka kabla ya makosa kufanyika

Kulingana na barua ya Amnesty International kwa rais wa Tanzania Suluhu Samia Hassan, waliokamatwa walifunguliwa “mashataka ya uongo yakiwemo kumuua afisa wa polisi.”

Barua hiyo inasema kwamba “walikamatwa hata kabla ya polisi huyo kuuawa na mashtaka yalibadilishwa mara nne na kupandikiziwa kesi ya kupanga kumuua polisi na kuongeza majina ya watu wengine kwenye orodha ya watu wanaozuiliwa na polisi.”

Mzozo kati ya wamaasai na Serikali ya Tanzania

Kulingana na serikali ya Tanzania, kuna umuhimu mkubwa wa kuhifadhi mazingira dhidi ya uharibifu unaofanywa na jamii ya wamaasai ambao ni wafugaji, katika mbuga ya kitaifa ya Serengeti.

Kwa sababu hiyo, serikali inawaondoa watu kutoka eneo la kilomita 1500 za mraba katika divisheni ya Loliondo na sehemu za Ngorongoro.

Zaidi ya watu 70,000 wamepangiwa kuondolewa sehemu hiyo pamoja na mifugo yao.

Kuna ripoti kwamba serikali imepanga kutoa sehemu hiyo ya ardhi kwa kampuni ya Ortallo kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu kwa ajili ya utalii.

Wamaasai ni watu wanaotegemea ufugaji hasa ng’ombe.

Watu wanaondolewa kwenye ardhi yao ya kijamii licha ya kuwepo kesi katika mahakama ya jumuiya ya Afrika Mashariki kutaka shughuli hiyo kusitishwa.

Msemaji wa serikali ya Tanzania Gerson Msigwa aliiambia Sauti ya Amerika kwamba “inachofanya serikali ni kulinda mazingira ni jukumu la kila serikali kufanya hivyo. Watu hao wanatoka kwa hiari bila kushurutishwa.”

Ardhi ya Loliondo ilipewa kwa Mwekezaji mwaka 1992

Kulingana na shirika la Amnesty International, serikali ya Tanzania ilitenga sehemu nzima ya Loliondo kwa kampuni kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu Mnamo mwaka 1992, kwa ajili ya uwekezaji wa kitalii.

Operesheni ya sasa ya kuwaondoa wamaasai ni jaribio la nne katika mzozo wa ardhi hiyo ambao umechukua zaidi ya muongo mzima.

Maafisa wa usalama waliwahi kujaribu kuwatimua wamaasai kutoka ardhi hiyo miaka ya 2009, 2013 na 2017. Operesheni ilifanyika katika vijiji vinne vya Ololosokwan, Oloirien, Kirtalo na Arash.

Mahakama ya jumuiya ya Afrika Mashariki ilitoa agizo kwa serikali kuacha operesheni hiyo, mnamo Septemba tarehe 26 mwaka 2018. Agizo hilo lilisitisha shughuli hiyo ya serikali “hadi uamuzi kamili utakapotolewa.”

Kesi iliwasilishwa na jamii ya wamaasai.

Uamuzi kamili wa mahakama ulikuwa umetarajiwa Juni tarehe 22 mwaka huu. Mahakama iliahirisha hadi Septemba 2022.

Msimamo wa serikali ya Tanzania

Msemaji wa serikali ya Tanzania Gerson Msigwa aliiambia Sauti ya Amerika, katika kipindi cha Kwa Undani kwamba “hakuna zuio lolote lililofanywa dhidi ya serikali kuendelea kufanya shughuli za serikali. Kinachofanyika Loliondo ni kuweka alama, na ni moja ya majukumu ya uhifadhi kuwaonyesha watu eneo linalopaswa kutumiwa na wananchi ni hili, na eneo hili limehifadhiwa," akiongezea kwamba "Umuhimu wa eneo la kilomita za mraba 1500 lililopo pale Loliondo ni kubwa na lenye maslahi ya taifa. Pale ndipo mahali kuna vyanzo vya maji vinavyohudumia hifadhi zetu nyingi zikiwemo Ngorongoro, Serengeti, Meyatu na mapori ya akiba.”

Msigwa alisisitiza kwamba “Hakuna taasisi ambayo inaweza ikaja ikaiamuru Tanzania kwamba usifanye kitu fulani....hatufanyi hivyo. Kama kuna shirika lina maoni au limefanya utafiti, utaratibu ni kwamba wanawasilisha maoni na utafiti wao kwa serikali. Haliwezi likaja na kuiamrisha nchi ya Tanzania. Hii ni nchi huru. Huwezi kutuamrisha. Huo utaratibu haupo.”

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG