Baadhi ya Wanasiasa na wachambuzi wanasema kiburi cha serikali kutokuwa sikivu ndio sababu iliyopelekea uzembe ulioathiri kutokea kwa vifo hivyo.
Serikali ya Tanzania inatupiwa lawama kwa kushindwa kudhibiti kwa haraka zoezi la uokoaji huku taswira ya walio wengi wakiona vifo vya watu 19 vilivyotokea vingeweza kuzuilika na marehemu hawakupaswa kupatwa na hayo ila ni uzembe tu wa Serikali.
James Mbatia Mwanasiasa Mkongwe nchini akizungumza na Sauti ya Amerika ametupa lawama zake kwa Serikali kutokana na mbinu zilizotumika za uokoaji ambapo amesema haziendani na uhalisia wa maisha ya sasa hali ambayo anaiona ni kushindwa kuwajali wananchi wanyonge.
Ajali hii imeibua simanzi na majonzi makubwa katika taifa kwa kupoteza watu katika ajali ambayo kama juhudi za haraka zingefanyika pengine maisha yangeweza kuokolewa na sasa kuzua mtazamo tofauti kwa walio wengi huku baadhi wakisema nguvu iliyotumika katika uokozi haiendani na wakati tulio nao.
Mkurugenzi wa Shirika la Kuelimisha na Kupambania haki za abiria Tanzania Ambakisye Mwakifwange akizungumza kwa masikitiko makubwa amesema ni jambo la kushangaza kwa ziwa kubwa la Victoria kukosa vyombo vya uokoaji pamoja na waokoaji wa kutegemewa.
Kwa upande wake Suleiman Majid ambaye ni Mdau wa Maendeleo kutoka Kibaha mkoa wa Pwani amesema kukosekana maandalizi ya serikali ya kupambana na majanga ndio sababu iliyopelekea kuwepo kwa vifo kwa kushindwa kusaidia kupeleka vitendea kazi kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Serikali imeombwa kubuni mikakati muafaka na njia sahihi za kujiweka tayari katika juhudi za uokozi endapo kunatokea majanga ambayo yanaweza kusababisha vifo vya wananchi.