Ramaphosa, ambaye alipigiwa upatu kuwa mtu anayepiga vita ufisadi baada ya utawala wa mtangulizi wake Jacob Zuma uliokumbwa na ufisadi, anakabiliwa na tuhuma kwamba alijaribu kuficha wizi mkubwa wa pesa katika shamba lake la kifahari.
Matokeo ya uchunguzi wa jopo huru, ambayo yalisema rais “anaweza” kuwa na hatia ya ukiukaji mkubwa na utovu wa nidhamu, yatagubika kikao maalum cha bunge mjini Cape Town leo mchana.
Wabunge wanatakiwa kuamua, kwa wingi wa kura, iwapo wanaendelea na utaratibu wa kumfungulia mashtaka ya kutaka kumuondoa madarakani.
Ramaphosa mwenye umri wa miaka 70 anaonekana atanusurika, baada ya wiki iliyopita kupata uungwaji mkono mwingine wa chama chake cha African National Congress (ANC) ambacho kinashikilia viti 230 kati ya 400 vya bunge, baada ya kuwasilisha ombi la kisheria la kutaka ripoti hiyo ya jopo huru ibatilishwe.