Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 08:58

Africa yaadhimisha miaka 57 tangu kuanzishwa OAU


Siku ya Afrika Mai 25
Siku ya Afrika Mai 25

Umoja wa Afrika (AU) unatoa wito kwa nchi wanachama kuongeza juhudi zao katika kusitisha migogoro na utumiaji silaha barani humo.

Umoja huo ukiadhimisha miaka 57 tangu kuanzishwa kwake Jumatatu Mei 25, umefanya mikutano kadhaa kupitia mtandao pamoja na tamasha la wanamuziki wa Afrika wakiwa nyumbani chini ya mada ya mwaka huu ya "Tunyamazishe silaha barani Afrika."

AU ilianda mkutano kwenye mtandao uliyoongozwa na Mwenyekiti wa sasa wa AU Cyril Ramaphosa, ambaye pia ni Rais wa Afrika Kusini pamoja na Mwenyekiti wa kamisheni ya Afrika, Moussa Faki Mahamat.

Viongozi hao waliwahutubia Waafrika kote duniani kwa lengo la kuhamasisha upya kauli mbiu hiyo.

Katika hotuba yake rais Ramaphosa amesema inabidi watu kutumia funzo lililopatikana wakati huu wa janga la corona na kusitisha migogoro barani humo.

Inaripotiwa kwamba idadi ya migogoro na uhalifu wa kutumia bunduki ilishuka sana pale nchi nyingi zilipo walazimisha wakazi kubaki nyumbani ili kupambana na ugonjwa wa COVID-19.

Kwa upande wake mwenyekiti Mahamat aliyeanzisha mfuko maalum mwezi Machi kuchangisha dola milioni moja kusaidia nchi za Afrika kuimarisha mifumo yao ya afya na hasa kuwasaidia wananchi kukabiliana na matatizo ya kiuchumi na kijamii kutokana na janga hilo, amewataka Waafrika kuchanga popote pale walipo.

Rais wa zamani wa Zambia Kenneth Kaunda alikuwa mgeni wa heshima akiwa kiongozi wa mwisho hai aliyekuwepo pale Umoja wa Nchi Huru za Afrika, OAU ulipoanzishwa mjini Addis Ababa tarehe 25 Mei, 1963.

Mbali na mkutano huo kulikuwa na mkutano wa baadhi ya viongozi wa Afrika Magharibi kuzungumzia mustakbal wa kiuchumi wa bara hilo pamoja na tamasha kuu la wanamuziki kutoka takriban kila nchi kupitia ukurasa wa Youtube ili kusaidia kuchangisha fedha kupambana na janga la corona.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Abdushakur Aboud, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG