Baraza la wawakilishi katika bunge la Marekani limepitisha mswaada wa mageuzi ya huduma za afya kwa kura 219 kwa 212 baada ya mjadala wa muda mrefu, mkali na uliojaa kila aina ya mivutano. Huu ni ushindi mkubwa kwa rais Obama ambaye alifanya mswaada wa afya kuwa swala lake kubwa katika kampeni yake na utawala wake.
Mswaada huo ni wa kwanza mkubwa wa aina hii katika kipindi cha miaka 40 nchini Marekani. Wabunge wote 178 wa chama cha Republican walipinga mswaada huo wakiungwa na mkono na wademocrat 34, lakini idadi hiyo haikutosha kuuzuia mswaada huo ambao serikali ya Obama inasema utatoa huduma za afya kwa mamillioni ya watu ambao walikuwa hawana bima za afya.