Marekani imezilaumu Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo – DRC – katika taarifa yake kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu duniani huku baadhi ya mashirika ya kimataifa yanayotetea haki za binadamu yakisema Marekani nayo inahitaji kuboresha pia rekodi yake.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuhusu haki za binadamu inaonyesha wazi kukiukwa kwa haki za binadamu duniani. Nchini Iran kwa mfano taarifa hiyo inatoa mifano ya watu waliokamatwa bila kufunguliwa mashtaka na pia wakiteswa wakiwa kifungoni.
Lakini baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu yanaituhumu Marekani kwa unyanyasaji wa aina hiyo hiyo kwa watuhumiwa waliokamatwa katika mapambano dhidi ya ugaidi. Mkurugenzi wa shirika la Amnesty International, T Kumar anasema kutotendewa haki kwa watuhumiwa waliomo katika gereza la Guantanamo Bay nchini Cuba kunaweza kufungua milango ya unyanyasaji wa hali ya juu.