Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy akiwa katika ziara ya siku moja Rwanda amekiri kuwa nchi yake ilifanya makosa wakati wa mauaji ya halaiki Rwanda mwaka 1994, lakini alisita kuliomba taifa la Rwanda samahani kamili.
Katika ziara yake ya kwanza Rwanda, Sarkozy alisema "kilichotokea hapa hakiwezi kukubalika, na kinailazimisha jumuiya ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Ufaransa, kutafakari makosa iliyofanya kutozuia mauaji yale."
Kiongozi huyo wa Ufaransa alikiri kwamba nchi yake kwa namna fulani ilifumbia macho hali iliyosababisha mauaji yale na haikuchukua hatua zozote kuyazuia ingawa ilikuwa na uhusiano wa karibu sana na Rwanda.
Hata hivyo, Rais Sarkozy hakufika hatua ya kuwaomba watu wa Rwanda samahani, na alionekana akijaribu kwa bidii kukwepa kuomba msamaha. Uhusiano wa Rwanda na Ufaransa umekuwa mbaya tangu mauaji hayo na hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo kutembelea Rwanda.