Dharuba kali iliyoleta zaidi ya nusu mita za theluji imesababisha kufungwa kwa shughuli katika mji mkuu wa Marekani wa Washington kwa siku ya tatu mfululizo, na kuwalazimisha wakuu wa mji na majimbo jirani kutangaza hali ya dharura.
Watalamu wa Idara ya Taifa ya Hali ya Hewa wanasema dharuba hii inatokana na El-Nino, hali inayosababishwa na kuongezeka kwa hali ya joto katika bahari ya Pacific katika kanda za joto na kubadilisha kabisa mwenedo wa upepo na hali ya hewa.
Hali hii inayotokea kila baada ya miaka mitatu hadi saba huweza ikasababisha vimbunga kama tulivyoshuhudia huko Asia ya Kusini mwaka jana, hadi hali ya ukame huko Afrika Mashariki, na dharuba ya majira ya baridi mashariki ya Marekani.
Theluji iliyomwagika kwa siku mbili na kufikia karibu sentimita 60 imesababisha kiasi ya nyumba na majengo ya bishara 218,000 kutokua na umeme. Watu pia wameshindwa kubaki majumbani na kulazimika kuondowa theluji mbele ya nyumba zao kwa siku nzima.
Watalamu wa hali ya hewa wanasema, dharuba hii ni ya tatu kwa ukubwa kwa jiji la Washington tangu ile ya mwaka 1922, lakini kwa kiwango cha kitaifa inatajwa kuwa ya nne kwa ukubwa ambapo ya kwanza ilitokea 1899.