Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 02, 2025 Local time: 23:12

Camara ataka kurudi Giunea


Kiongozi wa kijeshi wa Guinea aliyejeruhiwa, Kapteni Moussa Dadis Camara, anasema anataka kurudi nyumbani licha ya wito kutoka ndani ya Guinea na nje ya nchi kumtaka asijihusishe na siasa za nchini humo.

Maafisa wa Burkina Faso, wanasema Kapteni Camara alielezea matumaini yake baada ya kurudishwa kutoka hospitali moja ya Morocco kwenda mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou, Jumanne jioni.

Afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, William Fitzgerald, alisema Alhamisi kwamba Washington haitaki kiongozi huyo wa kijeshi kurudi Guinea. Makundi ya upinzani nchini Guinea na Ufaransa, ambayo ilitawala nchi hiyo zamani wanaonya kwamba kurudi kwa Camara kunaweza kuchochea vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mivutano ya kisiasa huko Guinea imeongezeka, tangu majeshi ya usalama yalipowauwa zaidi ya waandamanaji 150 kwenye mkutano wa upinzani mwezi Septemba.

Kapteni Camara alikuwa na mazungumzo na kiongozi wa Guinea anayekaimu madaraka, Jenerali Sekouba Konate na Rais wa Burkina Faso, Blaise Compaore. Bwana Compaore amekuwa akiongoza mazungumzo ya eneo yaliyolenga kumaliza matatizo ya kisiasa ya Guinea.

Wiki iliyopita, kiongozi huyo anayekaimu madaraka Jenerali Konate, aliomba kuunda serikali ya muda ili kupanga uchaguzi wa Guinea. Alisema upinzani utachagua waziri mkuu wa muda. Kapteni Camara alipata jeraha la kichwani baada ya kupigwa risasi na mmoja wa wasaidizi wake Disemba 3.

XS
SM
MD
LG