Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Kenya Moses Wetangula, alitangaza siku ya Jumatatu kwamba serikali ya Kenya inatafakari jinsi itakavyoweza kujibu kile inacho hisi ni ukiukaji wa itifaki ya kidiplomasia ulofanywa na serikali ya Marekani.
Bw Wetangula alisema,"ninataka kuhimiza hasa balozi wa Marekani, kwamba sina shaka hata kidogo kwamba amevuka mipaka ya itifaki ya kidiplomasia." Matamshi hayo yanafuatia hatua ya Marekani kuwapa maafisa 15 wa vyeo vya juu wa Kenya, barua inayowaonya kwamba hatua kali huwenda zikachukuliwa dhidi yao wakionekana kama wanazuia mageuzi muhimu ya serekali.
Barua zilitiwa saini na naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani anaeshughulikia masuala ya Afrika, Jonnie Carson, lakini balozi wa Marekani huko Nairobi, Michael Ranneberger anasema uwamuzi ulichukuliwa na maafisa wa vyeo vya juu wa serekali.
Hatu hiyo, ilimsababisha Rais Mwai Kibaki kumuandikia mwenzake wa Marekani, Rais Obama kueleza wasi wasi wake kwamba, Marekani inatoa vitisho vya kibinafsi kwa watumishi wa serekali kuhusiana na sera za ndani za utawala wake.
Nae waziri mkuu Riala Odinga, akiwa New York kuhudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa mataifa, alijibu hatua ya awali kwa kusema, Marekani inahaki ya kumnyima mtu yeyote ruhusa ya kusafiri kuingia nchini mwake, na ni sawa kuhimiza mageuzi yafanyike.
Baadhi ya wanasiasa, wakereketwa wa mageuzi na haki za binadam, na baadhi ya vyombo vya habari vimeunga mkono uwamuzi huo wa Marekani. Lakini serikali ya Kenya inaonekana imeanza kuchukua hatua kali zaidi ya kutetea haki zake za kufanya mageuzi yake bila ya kuingiliwa kati na mataifa ya kigeni.