Waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga atalihutubia Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York wiki hii juu ya kuharibiwa kwa msitu wa Mau.
Mzozo huu umendelea nchini Kenya kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita katika jimbo la Rift Valley, na Bw Odinga anatazamiwa kueleza juu ya hatua zinazochukuliwa na serikali yake kudhibiti uharibifu wa msitu huo ambao umeanza kuathiri chemchemi za maji katika kanda hiyo ya Afrika.
Siku kadhaa zilizopita waziri mkuu wa Tanzania Bw.Mizengo Pinda alitembelea Kenya na alikua na mazungumzo na serikali ya Nairobi kuhusu suala hili. Hasa ukizingatia kwamba uharibifu huo umeanza kuchangia kukauka kwa ziwa Natron na pia unaweza kusababisha athari kubwa katika uchumi wa Sudan na Misri, nchi zinazotegemea maji ya mto Nile kwa ajili ya shughuli za kilimo.