Rais Obama aliliachia bunge kuandika vipengele muhimu vya mpango wake
wa mageuzi ya bima ya afya, ambao hivi sasa unakabiliwa na upinzani
mkali kote nchini.
Bunge hivi sasa liko katika likizo yake ya
mwezi Augusti, lakini wabunge wamekuwa wakifanya mikutano katika kumbi
za miji, kote nchini, ili kusikia maoni ya watu kuhusu mageuzi hayo, na
wamesikia mengi, kutoka umati wa watu wanounga na wanopinga mpango huo.
Rais
Obama akiwa katika mikutano yake kuteetea mapendekezo yake amewambia
watu kwamba habari zinazotolewa kuhusiana na mpango wake kwa sehemu
kubwa haiambatani na mpango wenyewe.
“Kila mara tunapokaribia
kupitisha mswada wa mageuzi ya bima ya afya, walinda maslahi
wanaturudisha nyuma na kila kitu tulicho kubaliana. Wanatumia ushawishi
wao, na washirika wao wa kisiasa kututisha, na kupotosha wamarekani.
Wanafanya matangazo. Hivi ndivyo wanavyofanya siku zote hatuwezi
kuwaruhusu waendele kufanya hivi. Sio kwa wakati huu.”
Lakini kwa
sehemu fulani upinzani, unatokana na makadirio ya gharama, kutoka idara
huru, ya afisi ya hazina ya bunge la Marekani. Na kwa upande mwengine
baadhi ya watu wanasema hawajapata maelezo ya kutosha kuhusu mpango
huo, ili kuwawezesha kufanya uwamuzi muafaka.
Malengo mawili makuu
ya mpango huo wa mageuzi, ni kupanua bima hiyo ya afya, ili
kuwahudumia mamilioni ya wamarekani wasio na bima ya afya, na pili
kuweza kudhibiti kupanda sana gharama za huduma kwa wale ambao tayari
wenye bima ya afya.
Mpango wa bima wa uma, umependekezwa kuweza
kushindana na makampuni ya binafsi ya bima. Warepublican na wapinzani
wengine wanasema kwamba wazo la mageuzi la wademocrat, itapelkea kuwepo
na huduma za afya za mfumo wa kijamaa au kisocialisti.