Matokeo ya awali nchini Afrika Kusini yanaonyesha kuwa mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya chama tawala cha African National Congress, Jacob Zuma anaongoza kwa wingi wa kura, na waangalizi wa uchaguzi huo wanasema kwa ujumla uchaguzi umefanyika katika hali ambayo ni huru na ya haki.
Akiongea na Sauti ya Amerika kutoka Afrika Kusini, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Afrika, Dokta Salim Ahmed Salim, ambaye ni miongoni mwa wasimamizi wa uchaguzi huo, alisema Alhamis kuwa wameridhishwa na jinsi uchaguzi huo ulivyoendeshwa.
Dokta Salim alisema kuwa baadhi ya majimbo yalikuwa yameanza kutoa matokeo na kwamba chama tawala cha ANC kilikuwa kikiongoza kwa asilimia kubwa. Hata hivyo alisema kuwa kulikuwa na malalamiko kidogo kutoka upande wa upinzani kuwa hapakuwa na vifaa vya kutosha kupigia kura katika baadhi ya maeneo.
Lakini kwa ujumla alisema kuwa kasoro zilizojitokeza zilikuwa ndogo sana kiasi kwamba haziwezi kuathiri mchakato mzima wa uchaguzi. Dokta Salim aliwapongeza wananchi wa Afrika Kusini kwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura, na maandalizi mazuri yaliyofanywa na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo.