Kikao hicho cha mkutano maalum kinacho tathimini mafanikio na matatizo yanayoikabili serikali ya mseto nchini Kenya, kinasimamiwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, ambaye alipewa jukumu la kuwapatanisha Rais Mwai Kibaki na Raila Odinga, mara tu baada ya machafuko yaliyofuatia uchaguzi wa nchi hiyo.
Bwana Kofi Annan alikuwa amewaalika Rais Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga kuhudhuria mkutano huo wa Geneva, lakini viongozi wote wawili wamekataa mwaliko huo.
Badala yake serikali ya Kenya inawakilishwa na Naibu Waziri Mkuu, Musalia Mdavadi pamoja na mawaziri waliohusika na mazungumzo ya kuundwa serikali ya mseto ya nchi hiyo.
Baadhi ya watu wengine wanao hudhuria mazungumzo hayo ni pamoja na rais mstaafu wa Tanzania, Bwana Benjamin Mkapa.
Akihutubia kikao hicho, Bwana Kofi Annan alikumbusha jinsi alivyofika kuwapatanisha Rais Kibaki na Bwana Odinga, na kuwataja baadhi ya viongozi waliofika mara moja kusaidia baada ya kenye kuanza kuwaka moto.