Akifungua kesi hiyo katika mahakama ya Rwanda iliyokuwa imejaa watu, wakili wa Jenerali Nkunda alisema mteja wake alikamatwa na anashikiliwa kizuizini katika mazingira ambayo ni kinyume cha sheria.
Mbali na mazingira anaposhikiliwa Jenerali Nkunda, wakili wake amesema kuwa kiongozi huyo wa zamani wa waasi wa CNDP mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, alikamatwa akiwa kwenye mkutano nchini Rwanda ambapo alikuwa amealikwa.
Aidha wakili huyo alisema kuwa juhudi za kutaka kujua mahali anaposhikiliwa mteja wake hazikuweza kufanikiwa, na hivyo kumnyima Jenerali Nkunda haki ya kukutana na mwanasheria anaye mtetea.
Maelezo kuwa Nkunda alikamatwa akiwa kwenye mkutano rasmi na maofisa wa jeshi la Rwanda, yanatofautiana na taarifa ya jeshi la nchi hiyo, ambayo inasema kuwa alikamatwa wakati alipokuwa akijaribu kukimbia mapigano.