Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Philip Alston anaye chunguza mauaji hayo, alikutana na watu hao wawili mwezi uliopita. Alisema kuwa inasikitisha mno kuona kuwa wafanyakazi hao wa kutetea haki za binadamu, waliuawa hadharani jana katikati ya mji mkuu wa nchi hiyo Nairobi.
Oscar Kingara na John Oulu walipigwa risasi walipokuwa wamekwama kwenye msongamano wa magari, karibu na chuo kikuu cha Nairobi. Mwanafunzi mmoja pia alipigwa risasi na kuuawa wakati wa maandamano yaliyolipuka chuoni hapo.
Mauaji hayo yamefuatiwa na maandamano makubwa ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi, ambao baadhi yao walishuhudia mauaji hayo kwa sababu yalitokea karibu na chuo hicho.
Naye mchambuzi wa siasa ambaye pia ni mwandishi habari, Kasujaa Onyonyi, amesema matukio yanayoendelea nchini humo, yanaonesha kuwa serikali ya mseto ya nchi hiyo, imeshindwa kuimarisha utawala wa kisheria.