Rais Hu Jintao wa China yuko Mauritius ikiwa kituo chake cha mwisho katika ziara iliyomfikisha katika nchi nne za Afrika. Kabla ya kuwasili Mauritius alimaliza ziara ya siku tatu nchini Tanzania ambako China na Tanzania zilitiliana saini mkataba wa msaada wa dolla millioni 22 katika maswala ya kilimo na teknolojia ya mawasiliano. Rais huyo wa China pia alitembelea Mali na Senegal, Afrika Magharibi kwa ziara ya kuimarisha uhusiano kati ya China na mataifa ya Afrika.
Mkurugenzi mkuu wa baraza la kitaifa la biashara nchini Tanzania, Dan Mrutu anasema ni muhimu kwa Rais Hu kuhakikisha uhusiano kati ya nchi yake na Afrika unakuwa imara kwa sababu pande hizo mbili zimeshuhudia hivi karibuni uchumi kati ya China na Afrika ukikua kwa asilimia thelathini.
Mbali na Saudi Arabia ambayo inautajiri mkubwa wa mafuta, bwana Mrutu anasema nchi hizo za Afrika ambazo Rais Hu amezitembelea, zinafanya mageuzi makubwa ya kiuchumi na zina amani na rasilimali nyingi.