Morgan Tsvangirai ambaye ni kiongozi wa chama cha upinzani, Movement for Democratic Change (MDC), aliapishwa Jumatano na hasimu wake wa muda mrefu, Rais Robert Mugabe, katika sherehe ambazo zilihudhuliwa na viongozi kadhaa wa nchi za Afrika.
Wakati wa kuapishwa kwake, Bwana Tsvangira alionekana kujiamini na kuongea kwa sautia pale alipotamka maneno haya, "Mimi, Morgan Richard Tsvangirai ninaapa kuwa nitaitumikia vizuri na kwa ukweli Zimbabwe katika ofisi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Zimbabwe. Mungu nisaidie."
Wafuasi wa MDC na watu wengine waliokuwepo hapo walipiga makofi wakati Bwana Tsvangirai alipokula kiapo. Baada ya kumwapisha Tsvangira, Rais Mugabe alitoa hotuba na kusema atashirikiana na waziri mkuu mpya katika serikali ya umoja wa kitaifa.
Muda mfupi baada ya kula kiapo, Waziri Mkuu Tsvangirai aliwahutubia wafuasi wapatao elfu 10 katika mji mkuu wa nchi hiyo, na kusema machafuko ya kisiasa na unyanyasaji wa haki za binadamu lazima viishe mara moja.
Miongoni mwa watu waliohudhuli sherehe hizo ni Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki ambaye alisimamia mazungumzo kati ya ZANU-PF na MDC kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2007.