Maandamano yamefanyika kuelekea ubalozi wa Israel mjini Nairobi Kenya, kupinga mashambulizi yanayofanywa na majeshi ya Israel Ukanda wa Gaza. Maandamano hayo yalianza karibu na ofisi ya Waziri Mkuu na majengo ya bunge, na kuelekea ubalozi wa Israel.
Polisi waliokuwa katika magari maalum ya kutawanya waandamanaji walifanikiwa kuwatawanya vijana wa kiislam waliokuwa njiani kuelekea ubalozi wa Israel. Vijana hao wanaitaka serikali kumfukuza balozi wa Israel nchini Kenya, kutokana na kuhusika kwa nchi yake katika vita Ukanda wa Gaza.
Licha ya polisi kufanikiwa kuwatawanya waandamanaji hao, vijana hao wa Kenya wameahidi kuendelea na maandamano yao hadi pale serikali ya Israel itakapokuwa imekomesha mashambulio yake Gaza.