Mapambano makali yametokea nchini Kenya kati ya polisi na waandishi wa habari wanaopinga mswada wa serikali wa kusimamia na kudhibiti vyombo vya habari vya nchi hiyo.
Watu kadhaa wamejeruhiwa na waandishi wa habari sita walikamatwa na polisi walipokuwa wakishiriki maandamano ya kupinga muswada huo, lakini waliachiwa baadaye kwa dhamana ya dila 200 kila mmoja.
Hali imebadilika katika miji mbalimbali ya Kenya ambapo waandishi wa habari wa magazeti, redio na televisheni, wameahidi kuendelea na maandamano yenye lengo la kuishurutisha serikali kubadili mswada huo, kwa kubadili vipengele vinavyo dharilisha waandishi wa habari kama hatua ya serikali kuangamiza uhuru wa vyombo vya habari nchini humo.
Wakati huo huo, viongozi wa dini na makundi ya kutetea haki za binadamu wanamtaka rais Mwai Kibaki asiidhinishe mswada huo ambao tayari umepitishwa na bunge la Kenya, kwa maelezo kuwa hatua hiyo itarudisha nyuma nafasi ya demokrasia na uhuru wa kujieleza.
Mswada huo unatoa mamlaka kwa serikali kuvamia na kuharibu vifaa vinavyotumiwa na waandishi wa habari wanaodhaniwa kukiuka maagizo ya serikali.