Rais mteule wa Marekani Barack Obama ameungana na watu wanaotaka Gavana Rod Blagojevich wa jimbo la Illinois ajiuzulu kufuatia kashifa ya rushwa dhidi yake ambayo inatishia kudharilisha maandalizi ya kuapishwa kwa bwana Obama.
Msemaji wa Obama, Robert Gibbs alisema jana kuwa Blagojevich anatakiwa kujiuzulu kwa sababu itakuwa vigumu kufanya kazi yake ipasavyo katika hali hiyo.
Bwana Blagojevich anakabiliwa na mashitaka ya rushwa baada ya kukamatwa Jumanne kwa madai kuwa alikuwa akijaribu kuuza nafasi ya bwana Obama katika Seneti na kutaka kutoa upendeleo mwingine wa kisiasa ili aweze kulipwa fedha.
Waendesha mashitaka wa serikali kuu wanasema hakuna ushahidi wowote unaoonyesha rais mteule Barack Obama alikuwa na habari kuhusu juhudi za Gavana Blagojevich za kunadi kiti chake cha seneti.
Bwana Obama alizungumza kwa kifupi na waandishi wa habari siku ya Jumanne na kusema hakuwasiliana na Gavana au afisa wake, na kwa hiyo hakujua yaliyokuwa yakiendelea.