Wajumbe kutoka serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na waasi wa nchi hiyo, wamekutana kwa mara ya kwanza ana kwa ana mjini Nairobi kwa mazungumzo yenye lengo la kumaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe na mateso kwa wananchi wa nchi hiyo.
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa na rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, alisema kuanza kwa mazungumzo hayo jana, ni nafasi ambayo haitakiwi kuachwa ipotee.
Naye mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika, rais wa zamani wa Tanzania Benjamini Mkapa alisema, "Hii ni nafasi ya pekee na nadra sana, ya kuweza kupata ufumbuzi wa mgogoro wa Congo."
Aidha bwana Mkapa amesema wanachotaka ni kuhakikisha mapigano yanamalizika kabisa na misaada inawafikia waathiriwa wa mapigano hayo.
Waasi wanaodai kulinda jamii za watusi dhidi ya makundi yenye silaha mashariki mwa Congo, wamekuwa wakiomba kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na serikali kueleza kilio chao.