Mkutano wenye lengo la kutanzua matatizo ya usafiri wa mizigo Afrika mashariki, umemalizika leo katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali kwa kutoa mwito wa kuondolewa vizuwizi vingi vya barabarani, na ukaguzi mrefu wa forodha.
Mwenyekiti wa baraza la wafanyabiashara wa Uganda, Omar Kasim amesema tatizo kubwa wanalokabiliana nalo ni kuchelewa kwa mizigo katika bandari za Mombasa na Dar es Salaam, na pia kupanda kwa gharama za usafirishaji wa mizigo hiyo.
Bwana Kasim amesema tatizo lingine linalo wakabili wafanyabiashara wa Afrika mashariki, ni vituo vingi vya kupima uzito wa malori yanayobeba bidhaa kutoka bandari za Mombasa na Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa bwana Kasim, vituo hivyo ni vingi na wasafirishaji wa mizigo hiyo hulazimika kutoa hongo kuwezesha mizigo yao kusonga mbele na kulipa malipo mengine ambayo siyo ya lazima. Akitoa mfano, bwana Kasim amesema kutoka Mombasa hadi Kampala ambapo ni kilomita zipatazo 1400, kuna vizuwizi vya barabarani vipatavyo 47.
Mkutano huo wa siku tano umekubaliana kupunguza vizuwizi hivyo, au kuviondoa kabisa ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo.