Katika mjadala maalum uliopeperushwa hewani tarehe 9 Novemba mwaka 2008, wachambuzi wanazungumzia ushindi wa kihistoria wa mgombea urais Barack Obama, alioupata Novemba 4 siku ya uchaguzi nchini Marekani.
Wachambuzi wa maswala ya kisiasa, Profesa Charles Bwenge wa chuo kikuu cha Florida, na Profesa George Kakoti wa chuo kikuu cha NOVA, South Eastern Cha Florida, wanauelezea ushindi huo kuwa wa kihistoria kwanza kwa sababu mshindi ni m'marekani wa kwanza mweusi kuingia White House.
Wamarekani weusi na hata wahamiaji kutoka Afrika sasa wanatembea vifua mbele kufuatia ushindi huo. Wengi weusi kwa wazungu walibubujikwa na machozi ya furaha, kwani hisitoria ya ubaguzi wa rangi ingali inajidhihirisha hapa na pale, miaka mingi tangu kupigwa marufuku biashara ya utumwa.
Kwa wanaoishi Marekani, watu weusi wamekuwa na nafasi finyu za maendeleo, na siku zote wanajiona wako nyuma licha ya juhudi za kutokomeza ubaguzi wa rangi nchini hapa ulioota mizizi.
Katika mjadala huu wachambuzi wa maswala ya kisiasa ya Marekani wanaelezea changamoto zitakazomkabili rais mteule Barack Obama mara tu baada ya kuapishwa Januari 20 mwaka 2009.
Bwana Obama atarithi uchumi uliodorora na atakuwa na kibarua kigumu cha kujenga uhusiano bora na jamii ya kimataifa ambayo kutokana na vita dhidi ya Iraq imeelezea kutofurahishwa na Marekani.
Kwa waafrika na hasa nchi ya Kenya alikotoka baba yake Obama, furaha na matarajio hayana kifani. Bara la Afrika linatazamia kuwa karibu sana na utawala wa Barack Obama na kunufaika kutokana na biashara baina ya Afrika na Marekani.
Kwa baadhi ya wakenya, Ikulu ya Marekani ni kama ngazi moja juu ya ile ya Nairobi. Kampeni na njia alizopitia rais mteule Barack Obama ilikuwa ngumu, na wapinzani wake walimpiga vita wakisema jina lake la kati linaonyesha yeye ni muislam.
Lakini sivyo, Obama ni mkristo, na jina hilo alipewa na baba yake. Haina maana yoyote kuwa mtu ni wa imani fulani. Marekani inasema ni vumilivu kwa imani zote. Swali ni kama rais mteule Obama atalitumia jina lake la kati kujitambulisha pale atakapokula kiapo Januari 20 mwaka ujao. Kwa majibu ya swali hilo na mambo mengine, sikiliza mjadala huu maalumu kwa kubonyeza hapo juu.