Barack Obama alikuwa na ujumbe wa kawaida katika kinyang'anyiro chake cha miezi 21 kuingia White House, mabadiliko. Lakini Obama hakuzungumzia tu mabadiliko, aliyaonyesha.
Obama alisema, "Kwasababu ya kile tulichokifanya siku ya leo, katika uchaguzi huu, wakati huu muhimu, mabadiliko yamekuja."
Akiwa kiongozi wa kwanza mmarekani mwenye asili ya kiafrika kuingia White House, rais mteule Obama ameandika ukurasa mpya katika historia ya Marekani na ametimiza matarajio yaliyoko katika azimio la uhuru kwamba watu wote wameumbwa sawa.
Lakini njia ya Barack Obama kuelekea White House haikuwa kinyume na wengine katika historia ya Marekani. Obma kwanza na pengine ushindi muhimu ulipatikana katika mkutano wa wanachama wa Democratic mwezi Januari huko Iowa, uthibitisho kwamba mgombea mweusi huenda akawavutia wapiga kura weupe.
Njiani kuelekea kwenye historia hii, Obama alinufaika kutokana na dhoruba za kisiasa. Jinsi mwaka ulivyokuwa unakwenda, na ukusanyaji maoni ya umma ukionyesha kwamba wamarekani kwa kiasi kikubwa hawakubaliani na rais Bush na hivyo walikuwa wanataka nchi ichukue mwelekeo mwingine.
Mtaalamu wa mikakati ya kisiasa katika chama cha Democratic, Joe Trippi anasema, "Watu kwa kweli walikuwa wanataka mabadiliko. Walikuwa wamechoshwa na miaka nane ya George Bush. Na kwa kweli Barack Obama alilibaini hilo."
Mapema mwezi Septemba, Obama alikuwa nyuma ya mpinzani wake mrepablica, seneta John McCain katika ukusanyaji maoni. Lakini mzozo wa kifedha ulipokuwa mkubwa katikati ya mwezi Septemba, uchumi ulikuwa ni suala la kwanza kwa wapiga kura wengi, na lilibakia hivyo hadi siku ya uchaguzi.