Mawaziri hao walisema nchi zao zitafanya hivyo kwa misingi ya utawala wa sheria ili kuimarisha usalama wa kimataifa, kuendeleza ustawi wa uchumi, na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za baharini. Walitoa taarifa hiyo baada ya mkutano uliofanyika mjini Charlevoix, Canada.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya wamesisitiza kuwa usalama na ustawi wa baharini ni mambo muhimu kwa utulivu wa kimataifa, uimara wa uchumi, na ustawi wa mataifa yote duniani.
Zaidi ya asilimia 80 ya bidhaa za biashara ya kimataifa zinasafirishwa kwa njia ya bahari, na asilimia 97 ya mtiririko wa data duniani hupitia katika nyaya za chini ya bahari.
Mabadiliko katika njia za bahari yanahatarisha usalama wa chakula duniani, rasilimali muhimu, usalama wa nishati, usambazaji wa kimataifa, na ustawi wa uchumi.
Viongozi wa G7 wameonyesha wasiwasi wao kuhusu kuongezeka kwa athari zinazohatarisha usalama wa baharini, ikiwemo changamoto za kimkakati, vitisho vya uhuru wa meli kupita, na shughuli za usafirishaji haramu.
Katika mkutano huo walizungumzia kuongezeka kwa vitisho vya usalama katika maeneo ya baharini, ikiwemo ongezeko la mashambulizi ya kibiashara, wizi wa majini, na uharibifu wa mazingira ya bahari.
Katika muktadha huu, walitaja kuongezeka kwa vitisho kuhusu uhuru wa meli kupita katika maeneo kama vile huko South China Sea, Bahari ya Shamu na Bahari ya Black Sea, na kusisitiza umuhimu wa kulinda haki za meli kupita, kama ilivyoainishwa na sheria za kimataifa.
Aidha walijitolea kuongeza ushirikiano katika kulinda miundo mbinu ya nishati na mawasiliano ya chini ya bahari, ambayo ni muhimu kwa ustawi wa uchumi. Walielezea wasiwasi wao kuhusu madhara yanayotokana na uharibifu wa nyaya za mawasiliano chini ya bahari na miundo mbinu mingine muhimu ya baharini, ambayo inaweza kusababisha usumbufu katika mtiririko wa taarifa na nishati duniani.
Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa kupambana na uhalifu wa baharini, ikiwa ni pamoja na uharamia, wizi wa majini, na biashara haramu ya watu, wakionyesha kuwa uhalifu huu unahatarisha usalama wa baharini na biashara ya kimataifa. Walizungumzia juhudi za kupambana na shughuli hizi haramu kwa ushirikiano na nchi mbalimbali, ikiwemo azma ya kuzuia matumizi ya meli za kivita zisizo na usajili na zile zinazohusishwa na uhalifu.
Kwa upande mwingine, G7 walizungumzia kuhusu hatari zinazosababishwa na mashambulizi ya kigaidi katika maeneo ya baharini, kama vile mashambulizi ya Wahouthi kwenye bahari ya Shamu, ambayo yamehatarisha usalama wa meli za biashara na kuathiri biashara ya kimataifa.
Viongozi hao walielezea umuhimu wa kulinda haki ya meli kupita kwenye maeneo muhimu ya bahari kama vile Mlango wa Suez, na kushukuru juhudi zinazofanywa na operesheni za EU na Marekani katika kuhakikisha usalama wa njia za bahari za kimataifa.
Taarifa ya G7 pia iliangazia uharibifu wa mazingira ya bahari kutokana na shughuli za uvuvi haramu, zisizo ripotiwa, na kudhibitiwa, ambazo ni hatari kwa rasilimali za baharini na ustawi wa viumbe wa majini. Walielezea umuhimu wa kutumia teknolojia ya kisasa katika kufuatilia na kudhibiti shughuli hizi haramu, ikiwa ni pamoja na kupitia matumizi ya mfumo wa uchunguzi wa meli, ili kuhakikisha usalama wa mazingira ya bahari.
Viongozi wa G7 pia walisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kulinda usalama wa baharini. Walizungumzia jukumu la Umoja wa Mataifa katika kutoa miongozo ya kisheria kuhusu matumizi ya bahari na maeneo ya kipekee ya kiuchumi, na kuhimiza ushirikiano na nchi nyingine za mashariki na kaskazini mwa Afrika, na Umoja wa Afrika, ili kuboresha usalama wa baharini kwa jumla.
Taarifa ya G7 ilitoa wito kwa nchi zote duniani kuungana na kutoa msaada wa dharura ili kulinda usalama wa maeneo ya bahari, kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za bahari, na kulinda biashara na usafiri wa kimataifa dhidi ya vitisho mbalimbali.
Forum