Jaji wa Mahakama ya Washington, Tanya Chutkan Jumatatu aliondoa mashitaka ya kuingilia matokeo ya uchaguzi wa rais wa 2020 dhidi ya Trump. Hatua hiyo ni kufuatia ushauri kutoka kwa mwendesha mashtaka maalum wa Marekani Jack Smith, aliyewasilisha waraka mahakamani, kwamba sera ya muda mrefu ya idara ya mahakama inaondoa mashitaka dhidi ya Rais aliyeko madarakani.
Kwenye ombi lingine kwa mahakama, Smith amesihi mahakama ya rufaa ya Atlanta iondoe Trump kwenye kesi ya rufaa iliyokuwa inasubiriwa. Waendesha mashitaka wa Atlanta awali waliwasilisha rufaa ya kutaka Trump aendelee na kesi ya tuhuma za kupatikana na nyaraka muhimu za serikali kwenye nyumba yake ya Florida baada ya kuondoka madarakani 2021.
Trump kupitia mtandao wa Truth Social amesema kuwa,” Kesi hizi pamoja na nyingine nyingi zililazimishwa na wala hazina msingi wowote na wala hazikufaa kuwepo kamwe.” Aliongeza kusema kuwa chama cha Demokratik kimetumia zaidi ya dola milioni 100 za walipa kodi, kupitia kesi dhidi yake kama mpinzani wao wa kisiasa.
Forum