Idara ya huduma za dharura ya Umoja wa Mataifa OCHA inasema inashirikiana na washirika wengine wa huduma za dharura kukabiliana na janga hilo.
Naibu mkurugenzi mkazi wa Idara ya Huduma za Dharura ya Umoja wa Mataifa, OCHA nchini Congo Suzanna Tkalec, akizungumza na Sauti ya Amerika Jumatatu Washington kwamba wanawake na wasichana katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri wanaendelea kukabiliwa na kiwango cha kutisha cha ghasia za kingono kutokana na kuzuka upya mashambulizi yanayofanywa na makundi yenye silaha yanayopambana pia na jeshi la serikali.
“Ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka MSF, inaeleza kwamba kesi zilizoripotiwa za wanawake na wasichana walokwende kupata huduma za afya kutokana na ubakaji na ghasia za kingono zimefikia elfu 90 mwaka huu. Hiyo ni chembe tu ya tatizo kamili kwani ghasia dhidi ya wanawake haziripotiwi kwa namna inavyostahiki,” amesema Tkalec.
Anasema hali hii inatokana na kwamba waathiriwa hawawezi kutafuta msaada wa kiafya au kuripoti juu ya unyanyasaji huu wa kikatili kwa kuhofia unyanyapaa katika jamii zao au kuogopa ulipizaji kisasi kwani watenda maovu wanaishi nao kwenye miji na makambi ya walokoseshwa makazi.
“Sehemu kubwa ya hali hii inatokana na kwamba wanawake na wasichana wako katika hali ya hatari daima kwenye maeneo ya migogoro. Msaada wetu wa kibinadamu kama nilivyotaja haukidhi hata kidogo mahitaji yaliyopo. Kwa mfano katika juhudi zetu za kutafuta fedha zinazohitajika kwa huduma za dharura kwa ajili ya mwaka huu pekee tumeweza kupata asili mia 38 ya mahitaji kamili,” amesema Tkalec.
Naibu mkurugenzi wa OCHA anatoa wito kwa jumuia ya kimataifa na hasa vyombo vya habari kuendelea kuzungumzia hali ya kibinadamu huko DRC kwani hali inazidi kuwa mbaya kwa watu milioni 2 laki 8 walokoseshwa makazi kutokana na ghasia zilizoanza mwaka jana pekee yake. Kwa ujumla kuna watu zaidi ya milioni 5 hivi sasa walokoseshwa makazi huko mashariki ya Congo kulingana na Umoja wa mataifa.
“Tunahitaji msaada na tuna wategemea nyinyi kuhakikisha suala la DRC linaendelea kutangazwa. Kwa sababu tunafahamu daima kuna mashindano kutokana na mizozo mipya inayojitokeza duniani na kuona suala la DRC likiendelea kusahaulika kwenye mizozo ya kimataifa.
Tkalec kwa upande mwengine ameipongeza Marekani kwa kuendelea kua mhisani mkuu kwa DRC na ameridhika na mazungumzo yake na viongozi wa Washiongton ambao wamehakikisha kwamba msaada wa Marekani utaendelea kutolewa.
Forum