Upepo mkali na theluji katika miji kuanzia kaskazini hadi kusini mwa Marekani umesababisha usafiri wa ndege kuwa mgumu na mashirika ya ndege kufuta karibu safari 5 700 za ndege siku ya Ijuma pekee yake.
Rais Joe Biden akizungumza na waandishi habari siku ya Alhamisi aliwaonya Wamarekani kuchukua tahadhari kutokana na baridi kali na kusafiri mapema ikiwa wana mipango ya kukusanyika pamoja na familia na marafiki kwa ajili ya Krismasi.
Rais Biden amebaki Washington kusherehekea Krismasi amesema hali ni ya hatari na kwamba amezungumza na maafisa wa Mamlaka ya Huduma za Dharura, FEMA, na Idara ya Taifa ya Hali ya Hewa juu ya mipango yao.
Hali hii ya hewa ambayo ni nadra na hutokea mara moja katika kizazi kulingana na watabiri wa hali ya hewa, imeathiri majimbo 26 ya Marekani kutokana na upepo mkali wa baridi unaokwenda kwa kasi ya kilomita 100 kwa saa hadi kufikia mpaka wa Mexico upande wa Kusini.
Hali hii imesababisha pia mafuriko na theluji nyingi katika majimbo ya kaskazini na baridi ya kugandisha maji inakumba majimbo ya mashariki na kuwaathiri watu milioni 240.
Watu 12 wameripotiwa wamefariki kutokana na baridi kali huku miji ikifungua vituo maalum kwa ajili ya watu wasio na makazi wanaoishi barabarani.
Karibu watu milioni 1.8 hawana umeme katika nusu ya majimbo ya mashariki pamoja na Texas siku ya Jumamosi kutokana na dhoruba kali, ambapo majimbo ya kusini yakiathirika zaidi.
Baridi hii kali inayotokea Bara la Arctic, inaiathiri pia Canada ambako shughuli nyingi zimesita kutokana na theluji nyingi kuwahi kutokea.