Shirika hilo la chakula la Umoja wa Mataifa, limesema kwamba limekuwa likikabiliana na athari za ukame nchini Somalia kwa kuhakikisha kwamba chakula cha msaada kinawafikia mamilioni ya watu.
Mkurugenzi wa WFP nchini Somalia Laura Turner, amesema kwamba kuna haja ya msaada wa chakula kuongezwa marudufu na kuwafikia watu milioni 4.2.
Alikuwa akizungumza mjini Mogadishu ambapo alisisitiza kwamba shirika la WFP linaendelea kutoa msaada wa chakula kwa idadi kubwa ya watu, na kwamba kiasi cha watoto na akina mama milioni moja wanatibiwa maradhi yanayotokana na utapiamlo.
Amesema kwamba kuongezeka kwa msaada wa chakula kwa sasa, ni hatua nzuri inayosaidia kuizuia Somalia kuingia katika hali mbaya ya ukosefu wa chakula.
Hata hivyo ameonya kwamba hali inaelekea kuwa mbaya zaidi.
“Tupo katika hali mbaya. Kama tulivyosema mwezi mmoja uliopita, iwapo hali hii itaendelea kuwa mbaya, namna tunavyotarajia kutokana na ukosefu wa mvua, hali itakuwa mbaya zaidi. Iwapo msaada wa chakula hautaendelea kuongezeka, hali itakuwa mbaya zaidi kabla ya mwaka huu kumalizika.”
Umoja wa Mataifa umetabiri kwamba ukame utaendelea hadi katika wilaya za Baidoa na Burhakaba eneo la Bay.
Watu milioni 6.7 kote nchini Somalia wanatabiriwa kukumbwa na uhaba mkubwa wa chakula kabla ya mwaka huu kumalizika.