Liz Truss atachukua nafasi ya Boris Johnson kama Waziri Mkuu wa Uingereza siku ya Jumanne akisafiri kumwona Malkia Elizabeth huko Scotland kabla ya kuteua mawaziri wa vyeo vya juu katika baraza lake la mawaziri ili kushughulikia mzozo wa kiuchumi na kuunganisha chama chake kilichogawanyika.
Truss alimshinda mpinzani wake Rishi Sunak katika upigaji kura wa wanachama wa uwongozi wa chama cha Conservative na kuahidi kupunguza kodi na kuwasaidia watu kulipa bili zao za nishati wakati Uingereza inakabiliwa na shida ya nishati inayoongezeka. “Asante kwa kuweka Imani yako kwangu kukuongoza na kujitoa kwa ajili ya nchi yetu nzuri, Truss alisema. Nitachukua hatua shupavu kutuvusha sote katika nyakati hizi ngumu, kukuza uchumi wetu na kuibua uwezo wa Uingereza”.
Atamrithi Boris Johnson ambaye alilazimika kutangaza kujiuzulu mwezi Julai baada ya kashfa iliyoshuhudia uungwaji mkono kwa utawala wake ukipungua na mawaziri kujiuzulu na kulazimika yeye kujiuzulu.