Prince Charles wa Uingereza na mkewe Camilla waliwasili Rwanda siku ya Jumanne.
Wanandoa hao wa kifalme wakilakiwa na maafisa waliposhuka kwenye ndege mjini Kigali, kabla ya sherehe za ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola.
Lakini mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Uingereza pia anawasili huku kukiwa na utata kuhusu mpango wa Uingereza kupeleka waomba hifadhi nchini Rwanda.
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson anasema mpango huo wa dola milioni 148 uliofikiwa na Rwanda utasambaratisha mitandao ya watu wanaofanya biashara ya magendo.
Lakini safari ya kwanza ya ndege ilisitishwa wiki iliyopita kwa amri ya Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.
Prince Charles, kulingana na ripoti za vyombo vya habari, alielezea kwa faragha mpango huo kama wa kusikitisha.
Yeye na Camilla, Duchess wa Cornwall, wametembelea Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari ya Kigali na kukutana na manusura wa ukatili wa 1994.
Pia wanatarajiwa kukutana na Rais wa Rwanda Paul Kagame na mkewe.