Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 16:30

Serikali ya Uganda imesema kwamba haitakopa kulipa mishahara


Rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Serikali ya Uganda imesema kwamba haitaongeza mishahara ya wafanyakazi licha ya tetesi za shinkizo za wafanyakazi wa uma kutaka nyongeza hiyo.

Katika kikao na waandishi wa Habari jijini Kampala, katibu wa kudumu katika wizara ya fedha Ramathan Ggoobi amesema kwamba wafanyakazi waliosomea sayansi kama walimu wa sayansi na wauguzi pekee ndiyo watakaopokea nyongeza ya mshahara katika bajeti yam waka 2022/2023.

Katika bajeti hiyo, walaimu wanaofunza masomo ya sayansi wametengewa shilingi bilioni 400 kwa ajili ya kuongezewa mishahara. Hii ni baada ya walimu hao kufanya mgomo kuanzia wiki iliyopita, wakisema mshahara wanaopokea haulingani na tajiriba yao Pamoja na kazi wanayofanya.

Ggoobi amesema kwamba “wafanyakazi wengine wa serikali wanaotaka nyongeza ya mshahara watalazimika kusubiri,” bila kusema hadi lini.

“Tutatekeleza nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi wa serikali kwa mpangilio na katika makundi. Tuna wenzetu wa usalama nao wanataka kuongezewa mshahara. Tuna wafanyakazi katika wizara na taasisi mbalimbali ambao pia wanataka nyongeza ya mshahara, sawa na polisi, maafisa wa magereza na kadhalika. Kwa hivyo tuna mpango wa kufanya hivyo lakini hatuwezi kukopa pesa kulipa mishahara. Uganda haitafanya kitu kama hicho kamwe,” ameongezea.

Wanasayansi hasa madaktari na wauguzi nchini Uganda wamegoma mara kadhaa wakitaka kuongezewa mishahara.

Mgomo wa walimu wa sayansi na tishio la maandamano ya raia

Walimu wanaofunza masomo ya sayansi wamekuwa katika mgomo wakisema ni lazima serikali ya rais Yoweri Museveni itekeleze ahadi ambayo amekuwa akitoa kila mara, ya kuongeza mishahara ya walimu hao.

Mara nyingi, Museveni amekuwa akiahidi walimu wanaofunza masomo ya sayansi kuongezewa mishahara, akisema kwamba ni vigumu kuwapata.

Wanaharakati wamekuwa wakiitisha maandamano nchini Uganda kulalamikia ongezeko ya gharama ya Maisha. Katika sherehe za siku ya wafanyakazi, Museveni alisema kwamba wanaolalamika kwamba gharama ya Maisha imepanda, wanastahili kutafuta mbinu mbadala za kuishi, akitoa mfano kwamba iwapo mtu ameshindwa kununua mkate, basi akule mihogo.

Wizara ya fedha inasisitiza kwamba haitaendelea kukopa na raia wa Uganda wanastahili kuishi Maisha wanayoweza kumudu.

“Deni letu ni la chini sana ukilinganisha na majirani wetu Afrika mashariki. Tumekopa sana kukabiliana na athari za janga la Corona na kujenga miundo msingi. Hatutaki kuendelea kukopa Zaidi ya uwezo wetu,’ amesema Ggoobi.

Deni la Uganda

Kulingana na benki kuu ya Uganda, deni la nchi hiyo limeongezeka na kufikia dola bilioni 20.8

“Kuna nchi nyingi nyingi ambazo zinakopa ili kulipa mishahara ya wafanyakazi wa uma. Hatutafanya hivyo,” amesisitza Ggoobi.

Licha ya manung’uniko ya raia wa Uganda kuhusu ugumu wa Maisha, Gggobi amesema kwamba raia wana chakula cha kukula na hivyo serikali haitatoa msaada wa chakula.

Besigye anaendelea kuzuiliwa nyumbani kwake

Polisi wanaendelea kushika doria nyumbani kwa mwanaharaki wa haki za kiraia Dkt. Kiiza Besigye baada ya kumkamata na kumrudisha nyumbani kwake, alipojaribu kuongoza maandamano ya kulalamikia kuongezeka kwa gharama ya Maisha nchini Uganda.

Karibu wiki moja sasa, polisi wamezingira nyumbani kwa Besigye kuhakikisha kwamba hatoki na yeyote anayetaka kumuona lazima ajiandikishwe kwa maafisa wa polisi walio na kitabu maalum kwenye lango kuu la kuingia nyumbani kwake.

Hatua ya polisi kukita kambi nyumbani kwa Besigye, imepelekea bunge la taifa kuandaa kikao maalum, na kuagiza serikali kuhakikisha kwamba polisi hao wanaondoka mara moja.

Spika Anita Among, aliungana na wabunge wa upinzani na kulaani namna maafisa wa usalama walivyomkamata na Besigye May 12, na namna wanavyoendelea kushika doria nyumbani kwake, akisema kwamba “ni makos asana na uvunjaji wa haki za kibinadamu”.

Mkurugenzi mkuu wa UNAIDS awataka polisi kuondoka nyumbani kwa Besigye

Naye Mkurugenzi mkuu wa shirika la umoja wa mataifa linalopambana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi Winnie Byanyima, ambaye ni mke wa Dr. Kiiza Besigye ametaka polisi kuondoka nyumbani kwake haraka iwezekanvyo.

“Polisi hawastahili wanavunja haki za Beisgye. Tafadhali achene kuvunja sheria na muondoke nyumbani kwangu.”

Byanyima amesema kwamba hatua ya polisi haiwezi “kuvumiliwa.”

Polisi wa Uganda wametoa taarifa wakisema kwamba “maandamano anayoitisha Beisgye kulalamikia kuongezeka kwa gharama ya Maisha, yatavuruga haki za watu wengine ikiwemo kutatiza usafiri wa magari, kutatiza amani, kutokea wizi, na vurugu mjini.”

Polisi wamefunga barabara za kwenda kwa Besigye. Idadi kubwa ya polisi wa kuzuia ghasia wameshika doria katika sehemu anayoishi na kwa majirani wake.

Kuna amri ya mahakama iliyotolewa mwaka uliopita, kupiga marufuku polisi kutomzuilia Besigye nyumbani kwake.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG