Asilimia 66 ya waliojibu ukusanyaji maoni wa kituo cha televisheni ya CBS News iliyotolewa Jumapili walisema demokrasia kwa kiasi fulani au inatishiwa sana, huku asilimia 33 wakisema demokrasia iko salama.
Ukusanyaji maoni umejiri siku chache kabla ya maadhimisho ya shambulio la Januari 6 kwenye bunge la Marekani mwaka uliopita, ambapo wafuasi wa aliyekuwa rais wa wakati huo Donald Trump, walivamia jengo la bunge wakati wabunge walikuwa katika kikao cha kuhalalisha ushindi wa Joe Biden.
Miongoni mwa waliohojiwa katika kura ya maoni, asilimia 83 walisema hawakubaliani na watu walioingia kwa nguvu ndani ya bunge.
Wengi wanaona kwamba vitendo vya waliohusika katika shambulio la Januari 6, ilikuwa jaribio la kuipindua serikali ya Marekani, na kujaribu kufuta matokeo ya uchaguzi ili Trump asalie madarakani, na pia wanaona kwamba maandamano hayo ya Januari 6 yalichukuwa mwelekeo mbaya.