Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 00:31

Askofu Desmond Tutu afariki


Askofu mstaafu Desmond Tutu aliyeaga dunia Jumapili 26 Desemba 2021.
Askofu mstaafu Desmond Tutu aliyeaga dunia Jumapili 26 Desemba 2021.

Askofu mstaafu wa kanisa la Kianglikana, Desmond Tutu wa Afrika Kusini, ambaye alikuwa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 90.

Rais wa nchi hiyo Cyril Ramaphosa alitoa tangazo hilo Jumapili na kumtaja Tutu kama kiongozi wa kidini aliyekuwa mfano bora wa kimaadili katika taifa hilo.

"Kifo hiki ni ukurasa mwingine wa majonzi kwa taifa letu wakati tukimuaga kiongozi huyo wa kizazi maalum cha ukombozi," alisema Ramaphosa.

Hata hivyo, kilichosababisha kifo chake hakikubainika mara moja.

Tutu alipewa Tuzo ya Amani ya Nobel mnamo mwaka wa 1984 kwa kuongoza mapambano yasiyo ya vurugu dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi, wakati ambapo viongozi wakuu wa kisiasa kama Nelson Mandela walikuwa gerezani.

Lakini mapambano hayakuishia hapo. Hata baada ya kuondolewa kwa utawala wa ubaguzi wa rangi, Askofu Tutu aliendelea na harakati zake akikosoa mapungufu ya utawala wa watu weusi wa Afrika Kusini na kuwasuta wale waliohusika katika visa vya ukiukwaji wa haki za binaadamu popote duniani.

Atakumbukwa pia kwa kuanzisha kauli maarufu ya “Rainbow Nation”, yaani taifa la rangi ya upinde wa mvua, akimaanisha Afrika Kusini wakati Nelson Mandela alipokuwa rais wa kwanza mweusi nchini humo.

Kufuatia ripoti kuhusu kifo cha mtetezi huyo wa haki na uhuru, risala za rambirambi zilimiminika kutoka pembe zote duniani.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alimtaja Tutu kama mfano bora wa kuigwa.

"Kifo cha Askofu Tutu siyo tu pigo kwa Afrika Kusini bali kwa bara nzima la Afrika ambako anaheshimika na kuenziwa kama mtetea amani na maridhiano," alisema Kenyatta kupitia taarifa.

Justin Welby, Askofu mkuu wa kanisa la Anglikana wa Canterbury, alimtaja Tutu kama "mtu wa maneno na vitendo."

Tutu alizaliwa mnamo mwaka wa 1931 katika kijiji cha Mpilo, na alipata umaarufu mwingi kwani pamoja na kushinda tuzo ya amani ya Nobel, pia aliteuliwa kama menyekiti wa tume ya kitaifa ya maridhiano katika moja ya nchi ambazo zimeshuhudia viwango vya juu zaidi vya unyanyasaji na ukiukaji wa haki za binadamu kwa misingi ya rangi.

-AFP imechangia ripoti hii

XS
SM
MD
LG