Serikali ya Korea kusini imesema kwamba itatoa msamaha maalum kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Park Geun-hye, anayetumikia kifungo cha muda mrefu gerezani kwa makosa kadhaa ya ufisadi.
Wizara ya haki imesema kwamba Park, ambaye alikuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Korea kusini, atasamehewa katika hatua ya kuimarisha umoja wa kitaifa wakati nchi hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa kutokana na janga la virusi vya Corona.
Akizungumza mjini Seoul, waziri wa sheria Park Beom-kye, amesema kwamba Park atapewa haki ya kupiga kura, lakini hataruhusiwa kugombea nafasi yoyote ya uongozi.
Park, ambaye ni binti wa aliyekuwa kiongozi wa kiimla wa nchi hiyo Chung-hee, alikamatwa na kufungwa gerezani mnamo mwaka 2017 baada ya kuondolewa madarakani kutokana na kashfa za ufisadi zilizopelekea maandamano makubwa barabarani.