Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 22:45

Virusi vya Omicron vinaenea kwa kasi sana lakini sio hatari – mwanasayansi wa Kenya


Prof Walter Jaoko, Mtafiti wa sayansi katika chuo kikuu cha Nairobi Kenya na mtafiti katika taasisi ya KAVI
Prof Walter Jaoko, Mtafiti wa sayansi katika chuo kikuu cha Nairobi Kenya na mtafiti katika taasisi ya KAVI

Mwanasayansi wa Kenya Prof Walter Jaoko amesema kwamba aina mpya ya virusi vya corona Omicron havina nguvu sana ikilinganishwa na aina ya Delta au virusi aina ya kwanza.

Katika mahojiano na idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika VOA katika kipindi cha Kwa undani, Prof Jaoko wa chuo kikuu cha Nairobi, amesema kwamba utafiti ambao umefanywa kufikia sasa, unaonyesha kwamba wagonjwa wa Omicron hawahitaji kulazwa hospitalini na wanaweza kupata nafuu baada ya mda mfupi wakiwa nyumbani.

“Habari ambazo tuko nazo za utafiti wa kisayansi zinaonyesha kwamba hivi virusi vya Omicron sio hatari sana kulinganisha na vile vilivyotangulia. Wagonjwa ambao wameambukizwa Afrika kusini hawana dalili za kuugua kama ilivyokuwa na corona ya awali hata kama Delta. Uhakika tulio nao ni kwamba Omicron sio hatari zaidi kuliko Delta lakini tuna uhakikika kwamba Omicron kinaenea kwa kasi sana kuliko Delta.” Amesema Prof Jaoko.

Jaoko anasema kwamba ni kawaida ya Virusi kubadilika badilika kwa sababu za kisayansi, baadhi vinaweza kuwa hatari na baadhi kukosa makali.

“hivi virusi vya Corona huwa vinabadilika. Hiyo ndio hali ya virusi hivi. Kile kinachoweza kuzuia virusi hivi kubadilika ni pale maambukizi yanapokoma. Kama maambukizi yataendelea, basi virusi vitaendelea kubailika.” Amesema Prof Jaoko akiongezea kwamba “Kubadilika kwa virusi vya Corona haina maana kwamba vinakuwa hatari zaidi. huenda hata kubadilika huku kukawa kwamba corona sio mbaya zaidi ikilinganishwa na ile ya kwanza.

Mwanasayansi huyo amesema kwamba mataifa ya Afrika yataendelea kuripoti maambukizi ya juu kutokana na aina mpya ya virusi vya Corona Omicron, kwa sababu ya idadi ndogo ya chanjo inayotolewa kwa watu.

“Wakati nchi nyingi duniani zinatoa chanjo kwa wingi ispokuwa Afrika ambapo wato wanasita kupokea chanjo, haya mabadiliko ya Corona yataendelea kupatikana hapa Afrika. Nchi Tajiri zisiangalie tu watu wao na kuwapa chanjo. Wahakikishe kwamba dunia nzima, watu wamepewa chanjo.”

Prof Jaoko ameonya kwamba japo Omicron sio hatari sana, kuna uwezekano mkubwa kwamba iwapo maambukizi hatadhibitiwa, kunaweza kutokea aina hatari ya Corona zaidi ya imeshuhudiwa kufikia sasa.

“Haya mabadiliko yanaweza kuleta corona mbaya zaidi na huenda itakuwa imetoka Afrika ambapo watu hawataki kupokea chanjo na itaenea hadi ifike hizo nchi za magaribi.”

Wanasayansi wanasema kwamba si kweli kwamba Omicron imepatikana kusini mwa Afrika inavyodhaniwa lakini ni kwamba imegunduliwa kusini mwa Afrika.

Shirika la afya duniani limesema kwamba hakuna sababu yoyote ya nchi kuanza kuwekea zingine vizuizi vya usafiri, hasa nchi za Afrika. Cha muhimu ni nchi kutoa chanjo kwa raia wake kwa wingi ili kuzuia maambukizi.

“Kuna watu wamegunduliwa kuambukizwa Omicron Uingereza na hawajawahi kusafiri nje ya Uingereza wala kukutana na msafiri kutoka kusini mwa Afrika. Hii ina maana kwamba kuna Omicron nchini mwao baada ya virusi kujibadilisha. Na nchi nyingi zina wagonjwa wa Omicron ambao hawajasafiri nje ya nchi.” Amesema Prof Jaoko.

Hakuna utafiti umebaini iwapo chanjo ya sasa inaweza kukabiliana na virusi vya Omicron lakini wanasayansi wanaeleza wasiwasi ya idadi ndogo ya watu wanaopokea chanjo hasa Afrika.

“Afrika inahitaji watu wapewe chanjo. Kama kuna maambukizi kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwingine, mabadiliko ya virusi vya Corona yataendelea.

Afrika ndilo bara kote duniani lenye idadi ndogo zaidi ya watu ambao wamepewa chanjo dhidi ya virusi vya Corona. Wanasayansi wanasema kwamba virusi vya Corona vitaendelea kubadilika kwa sababu ya watu kukosa kupokea chanjo.

Baadhi ya wanasaansi wanapendekeza kwamba jinsi ilivyo na chanjo dhidi ya kifua kikuu, ndivyo inavyostahili kuwa na virusi vya Corona, kwamba Chnajo dhidi ya Corona iwe ya lazima kote duniani.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG