Msemaji wa Polisi Fred Enanga, ameambia waandishi wa habari jijini kampala kwamba Isma Kiyemba, mwenye umri wa miaka 24 amekamatwa katika Kijiji cha Makandwa, mtaa wa Kajjansi, wilayani Wakiso, karibu na Kampala.
“Baada ya kukamatwa, polisi wamefanya msako nyumbani kwake na kupata vifaa kadhaa vinavyotengeneza vilipuzi, ikiwemo kemikali, nyaya za shaba, batri, misumari na vinginevyo”, amesema Enanga, akiongezea kwamba “kadi kadhaa za benki, kadi za simu na vifaa kadhaa vinavyotumika kutengeneza vilipuzi hatari vimepatikana”.
Polisi wamesema kwamba mshukiwa huyo ndiye aliyetengeneza kilipuzi kilichtumika kulipua basi la kampuni ya Swift safaris, wiki chache zilizopita.
Kulingana na polisi, mshukiwa alipatikana akitengeneza kilipuzi kwa kufuata maagizo ya kamanda wa kundi la ADF.
“Tuna taarifa kwamba aliandikiswa katika kundi la ADF katika mtaa wa Lweza na Imam Sulaiman Nsubuga anayetafutwa na vyombo vya usalama. Wakati tumemkamata, alikuwa na maandiko kuhusu anayotaka yafanyike atakapokufa, Pamoja na maandishi ya namna atakavyotekeleza mashambulizi.”, amesema Enanga.
Kundi la ADF, lenye ushirikiano na kundi la kigaidi la Islamic state, limeshutumiwa kutekeleza mashambulizi kadhaa nchini Uganda na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Jehsi la Uganda liliingia DRC siku moja iliyopita, kuwasaka waasi wa ADF.