Wanaharakati wa upinzani nchini Cuba leo wameitisha maandamano kwa ajili ya mabadiliko nchini humo. Hata hivyo serikali imeonya kwamba haitavumilia wapinga mapinduzi na vitendo vya ugaidi wakati wa maandamano hayo ambayo serikali inaamini ni sehemu ya mpango wa Marekani kuingilia kati masuala ya Cuba.
Waziri wa mambo ya nje wa Cuba Bruno Rodriguez ametaja maandamano ya leo Jumatatu kama operesheni ya kudhoofisha usalama iliyoundwa Washington.
Wafuasi wa upinzani wa Cuba wanapanga pia kufanya maandamano katika maeneo mbali mbali ya dunia ikiwemo mjini Miami hapa Marekani, ambayo ni makazi ya raia wengi wa Cuba.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, Jumapili ametoa wito kwa serikali ya Cuba kuheshimu haki za Wacuba, kwa kuwaruhusu kukusanyika kwa amani na kutumia sauti zao bila hofu ya ulipizaji kisasi wa kimabavu wa serikali, na kuacha wazi mtando wa internet na mawasiliano ya simu ili habari zisambae kiurahisi.